MUZIKI

SIKU chache baada ya Mahakama ya Kisutu kumwachia mtu aliyedaiwa kumteka na kumtesa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, serikali imemshukia daktari huyo na kudai ndiye chanzo cha kukwama kwa dola kukamata watu waliomteka.

Jana Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Eliazer Feleshi, alidai kuwa vyombo vya dola vimeshindwa hadi sasa kuwakamata waliohusika katika shambulio hilo kutokana na Dk. Ulimboka kukwepa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

Feleshi ambaye jana aliambatana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, alidai lawama zinazosukumwa kwa Jeshi la Polisi kwa madai ya kushindwa kuwakamata waliomtendea unyama daktari huyo hazina msingi, kwa kuwa mhusika mwenyewe hajafika polisi, licha ya kuitwa mara nyingi kutoa maelezo.

Alisema kama Dk. Ulimboka angetoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kungekuwa na mafanikio makubwa katika kuwasaka na hata kuwatia mbaroni waliohusika katika unyama huo.

“Kila mara mmekuwa mkilaumu polisi wanashindwa kukamata wahalifu lakini tutakamataje kama wenye ushahidi hawataki kutoa ushirikiano?

Kwa mfano mdogo tu ni ‘ishu’ (suala) ya Dk. Ulimboka, hadi leo hajatoa taarifa lakini polisi wanaendelea kusakamwa na kutukanwa tu,” alisema.

Hata hivyo, wakati Feleshi akitoa kauli hiyo, Dk. Ulimboka katika andiko lake alilolitoa mara tu baada ya kurejea nchini kutoka Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya matibabu, alimtaja mtu anayeaminika kuwa mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyemteka na kumtesa.

Ulimboka akimtumia Wakili Nyaronyo Kicheere alisema Ighondu na wenzake ni mhusika mkuu katika unyama aliofanyiwa, kauli ambayo imekanushwa mara kadhaa na serikali.

Mapema wiki hii, raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka aliachiwa na Mahakama ya Kisutu baada ya DPP Feleshi kumfutia shitaka. Hata hivyo Mulundi alikamatwa tena na sasa amefunguliwa mashitaka ya kutoa maelezo ya uongo kwa polisi.

Wakati DPP akisema hayo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, jana aligoma kuzungumzia shinikizo la kumtaka ajiuzulu kutokana na kukithiri kwa matukio ya raia kumwagiwa tindikali, badala yake amewataka Watanzania kuwa na ushirikiano wa pamoja kukabiliana na uhalifu huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, (IGP) Mwema alishindwa kukubali kujiuzulu wadhifa huo na badala yake alitoa majibu ya jumla huku akiwataka Watanzania kubadilika na kuona suala la kulinda raia na mali zao ni jukumu la kila mmoja na si kazi ya polisi pekee.

Mkuu huyo alisema kuwa Watanzania lazima waelewe kuwa suala la ustawi wa jamii linatokana na uwepo wa amani na utulivu. “Nchi hii si ya mtu mmoja bali ni ya kila Mtanzania, inashangaza kuona asilimia 89 ya Watanzania wanaona suala la kulinda raia ni la polisi, si kweli ni lazima tubadilike,” alisema.

Alisema kuwa jukumu la utu lipo pale pale, hivyo kama taifa wana dhamana ya kuhakikisha suala la matumizi mabaya ya tindikali na dawa za kulevya linakomeshwa.

Mwema alisema kuwa wanalaani vitendo vibaya na vya kikatili vinavyofanywa na mtu mmoja mmoja ambavyo vinaleta hofu kwa jamii.

Alisema kuwa juhudi mbalimbali zinafanywa kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa na hata kumalizwa kabisa. “Tumeamua kuja na mkakati wa pamoja kwa kuwa sasa matukio ya umwagiaji tindikali umeshamiri na hatuwezi kusubiri adhurike mtu mwingine, bali tusaidiane wote kwa pamoja kukomesha haya,” alisema.

Alisema kuwa lengo la kutengenezwa kemikali hiyo haikuwa kutumika vibaya au kumdhuru binadamu, bali ni muhimu kwa ajili ya vyombo vya usafiri na maabara.

“Hata kisu ukiangalia kimetengenezwa kwa ajili ya mambo ya msingi, lakini kikitumika vibaya kinaweza kudhuru watu,” alisema.

Huku akionyesha hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo bila kutaja jina, alisema kuwa ofisa wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mmoja amesimamishwa kazi baada ya kudaiwa kuruhusu kupita kwa mabegi tisa ya dawa za kulevya yaliyokamatwa Afrika Kusini mwezi uliopita.

Mwema alisema kuwa ni muhimu wananchi wakatoa taarifa mapema pindi waonapo mwenendo mbaya wa matumizi ya tindikali hiyo, kwa kuwa ni uhalifu mpya.

“Wananchi ndio waathirika wa kwanza, ni vema wakatoa taarifa mapema ili hatua ziweze kuchukuliwa, maana vyombo vya dola pekee haviwezi kuhimili jambo hilo,” alisema.

Matukio ya kumwagiwa tindikali kwa sasa yameshamiri nchini kufuatia baadhi ya raia kupata ulemavu na wengine vifo, huku Julai 19, mwaka huu mmiliki na mfanyabiashara maarufu wa maduka ya Home Shopping Centre, Said Mohammed Saad, akivamiwa na kumwagiwa maji usoni yanayodhaniwa kuwa ni tindikali.

Ikiwa ni takriban wiki mbili tangu kutokea kwa tukio hilo, juzi wasichana wawili raia wa Uingereza waliofika visiwani Zanzibar kujitolea kufundisha somo la Kiingereza walimwagiwa tindikali majira ya saa 1:15 usiku, Mtaa wa Shangani eneo la mji Mkongwe.

Hata hivyo wasichana hao walisafirishwa jana kwenda nchini Uingereza kwa ajili ya matibabu zaidi.

Mwaka 2007 Mkurugenzi wa Halihalisi Publishers, Said Kubenea, alimwagiwa tindikali, hatua inayomlazimu kwenda nchini India mara kwa mara kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Mwaka 2011 wakati wa uchaguzi wa ubunge Jimbo la Igunga, Musa Tesha, alimwagiwa tindikali, huku mkoani Arusha, wilayani Arumeru, Sheikh wa wilaya hiyo, Said Juma Makamba, alijeruhiwa kwa kumwagiwa usoni kimiminika kinachoaminika kuwa tindikali.

Wakati Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, Novemba mwaka jana alimwagiwa tindikali.

Mkemia Mkuu wa Serikali

Katika kikao cha jana, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyere, alipiga marufuku usafirishaji wa tindikali bila kibali na kuagiza wahusika kutunza kumbukumbu kuonyesha ukali wa tindikali na kutoa mrejesho wa kiasi walichouza kuanzia mwezi huu.

Alisema kuwa wasafirishaji wanapaswa kuwa na vibali kisheria ambavyo vimetolewa na ofisi yake.

Profesa Manyere alisema kuwa wauzaji wa rejareja ni lazima wawe wamesajiliwa na wanapaswa kutoa taarifa za mauzo wanayofanya kila baada ya miezi mitatu kuanzia sasa.

Alisema kuwa kuanzia sasa wamiliki wa vyombo vya usafiri hawaruhusiwi kuchukua kemikali hiyo na kwenda nayo nyumbani badala yake wapeleke magari yao. “Wale wa lita moja moja hawaruhusiwi kuuziwa bali itapaswa kuuzwa kuanzia lita tano na kuendelea,” alisema.

Source:Mtanzania Daima

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...