Takriban waumini 44 wameuawa kwa kupigwa risasi
wakiwa msikitini Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, kwa mujibu wa maafisa
wa jimbo la Borno.
Mauaji hayo yalifanyika wakati wa maombi ya
asubuhi Jumapili , ingawa taarifa zimejitokeza Jumatatu , kutokana na
hitilafu ya mawasiliano kwani jimbo hilo liko chini ya sheria ya hali ya
hatari.Shambulizi lilifanyika katika mji wa Konduga, ulio umbali wa kilomita 35 kutoka mji mkuu wa jimbo hilo , Maiduguri.
Washambulizi wanasemekana kuwa wanachama wa kundi la wapiganaji la Boko Haram, ambalo liliwaua maelfu ya watu tangu mwaka 2009.
Gazeti la Daily Post, liliripoti kuwa watu wengine 26 walikuwa wanatibiwa kwa majeraha waliyopata wakati wa shambulizi hilo hospitalini Maiduguri.
Mwanachama wa kikundi cha vijana kinachotoa ulinzi kwa raia, aliambia shirika la habari la Associated Press, kuwa wapiganaji wao wannne waliuawa walipojaribu kutoa kilio cha kutaka usaidizi.
Raia wengine kumi na wawili, waliuawa katika kijiji cha Ngom kinachopakana na Maiduguri.
Rais Goodluck Jonathan alitangaza sheria ya hali ya hatari katika majimbo matatu Kaskazini Mashariki mwa nchi mnamo mwezi Mei wakati wanajeshi walipofanya operesheni dhidi ya wapiganaji wa kiisilamu.
Boko Haram linapigania eneo la Kaskazini mwa nchi likitaka kujitawala kwa kutumia sheria za kiisilamu.
Mwandishi wa BBC mjini Lagos, anasema kuwa wakati kundi hilo limekuwa likishambulia makanisa, pia limekuwa likishambulia misikiti.
Habari za mashambulizi hayo zilijitokeza wakati kanda ya video ya kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau, ilipotolewa akidai kundi hilo kuhusika na mashambulizi hayo ikiwemo kushambulizi dhidi ya vituo vya polisi na kambi za jeshi.
0 comments:
Post a Comment